Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amefunga mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa mkoa wa Kagera yaliyofanyika kwa siku tano katika ukumbi wa ELCT Hotel Bukoba Manispaa.
Mhe. Majaliwa amewataka viongozi hao kwenda kuyafanyia kazi maazimio na kutekeleza mipango na kuwataka kuwa weledi, waaminifu, na waadilifu kwa kila fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Viongozi katika Halmashauri zetu zote watumikieni zaidi wananchi msisubiri waje maofisini, sikilizeni changamoto zao, wapeni nafasi ya kuzungumza nanyi na nyinyi kumbukukeni mnatakiwa kuwajibika moja kwa moja kwa wananchi” amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajjat Fatma Mwasa kwa kuanzisha mafunzo hayo kwa viongozi na kutoa wito kwa Wakuu wa Mikoa Mingine ya Tanzania kuendesha mafunzo ili kuleta tija na ufanisi katika kazi zao za kila siku.
Vile vile katika hafla ya kufunga mafunzo hayo Waziri Mkuu amekabidhi tuzo kwa Wilaya ambazo zimefanya vizuri katika utendaji wa kazi na kutoa huduma kwa wananchi kwa mwaka 2022/2023 ambayo Wilaya ya Kyerwa imeshika nafasi ya kwanza na kufuatiwa na Wilaya za Missenyi na Ngara.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mkuu Mkoa wa Kagera Mhe. Hajjat Fatma Mwassa yalikuwa na lengo la kufanya tathmini ya hali halisi ya Mkoa wa Kagera na kupanga mwelekeo wa pamoja utakaoleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa na Wilaya, Wakuu wa Wilaya, Makatibu tawala Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Taasisi za Umma na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka katika Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Kagera yaliyoanza tarehe 18-22 septemba 2023.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved