Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa leo, Januari 13, 2026, imefanya kikao cha wadau wa Bima ya Afya kwa Wote kwa lengo la kuweka mikakati ya kuhamasishaji jamii kuelekea utekelezaji wa huduma hiyo, itakayozinduliwa rasmi hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Mussa Gumbo, amesema lazima tufahamu kwamba ugonjwa haupigi hodi ndio maana Serikali imekuja na bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha kila mwananchi anapata bima ya afya.
"Sera ya Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha ,hivyo nilazima tuweze kuwafikia wananchi na kuwaelimisha ili waweze kujiunga na kupata huduma ya bima ya afya " amesema Ndg. Gumbo.
Akielezea mkakati huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Dkt. Lewanga Msafiri, amesema kuwa huduma ya Bima ya Afya kwa Wote inatekelezwa chini ya Sheria Na. 13 ya mwaka 2023, Sura ya 365 ambapo mpango wa utekelezaji wake ikiwemo gharama za uchangiajia wa shilingi 150,000 kwa mchangiaji na wategemezi watano watakao hudumiwa kwa mwaka mzima.
Aidha ametoa rai kwa wajumbe wa kikao kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu na kuhamasisha Jamii ili waweze kuanza kuwekeza kidogo kidogo ili kuweza kujiunga pindi bima ya afya kwa wote itakapozinduliwa.

Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho wamesema wamepata uelewa mpana kuhusu Bima ya Afya kwa Wote na faida zake kwa kusema mpango huo utamwezesha mgonjwa kupata matibabu kuanzia ngazi ya zahanati hadi Hospitali za Rufaa na hivyo kupunguza gharama za matibabu na kupata huduma wakati wowote katika Vituo vya tiba bila kusumbuliwa.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kwa kuwakutanisha Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata zote, wajumbe wa Kamati ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT), Kamati ya Huduma za Afya ya Wilaya (CHMT), Maafisa Tarafa, Viongozi wa Dini na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Copyright ©2025, ICT Department Kyerwa District Council . All rights reserved.