Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka wananchi kuwatunza, kuwalinda na kuwaheshimu wazee kwa kuwa wao ni tunu na hazina ya Taifa ambayo tumepewa na Mungu.
Amesema hayo katika Sherehe ya Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Rubuga Kata ya Kitwechenkura Oktoba 18, 2025 ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa alikuwa Mgeni Rasmi wa sherehe hiyo.
"Nasikitika sana kuona kuna vijana wanawasumbua wazee, kuna vijana wanadiriki kuwadhuru wazee, wengine wanawapiga na wengine wanapelekea mauaji ya wazee na wengine wanawanyang'anya Mali zao," ameeleza Mhe. Msofe.
Aidha Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi wawatumie wazee kuchota maarifa na busara kutoka kwa wazee wakiwa bado wako hai na kusema hatasita kwachukulia hatua za kisheria watu ambao watawasumbua na kinyang'anya wazee haki zao.
Naye Mzee Ezekia Kanyonyi Katibu wa Baraza la Wazee Wilaya ya Kyerwa akisoma risala kwa niaba ya wazee, amemuomba mkuu wa wilaya kuimarisha ulinzi kwa wazee na mali zao pia wameomba kupatiwa matibabu bure pamoja na kutungwa sheria na sera zitakazo wasaidia wazee kuwa sehemu ya maamuzi katika ngazi mbalimbali.
Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani huadhimishwa ifikapo Oktoba 01 kila mwaka na kwa Wilaya ya Kyerwa yameadhimishwa tarehe 18 Oktoba yakiwa na Kauli Mbiu isemayo, "Wazee Tushiriki Uchaguzi Mkuu kwa Ustawi wa Jamii Yetu".
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved