Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kyerwa, Mwl. Ramadhani Marwa amefungua mafunzo ya siku mbili kwa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo vya kupigia kura ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 29, 2025.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Oktoba 26, 2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, yakiyohusisha washiriki wa Vituo vya Kata ya Kyerwa na Nyaruzumbura ambapo washiriki hao wameaswa kizingatia sheria, miongozo na kanuni watakazopewa katika mafunzo hayo.
Mwl. Marwa amesema, kuna vituo 11 vya mafunzo ya wasimamizi, ambapo jumla ya wasimamizi 1,872 watapatiwa mafunzo na kwenda kusimamia katika Vituo 608 katika kata 24 za Jimbo la Kyerwa, ambavyo vitatumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.
“Dhamana mliyopewa ya kusimamia zoezi la kupiga Kura na kuhesabu kura ni nyeti na muhimu kwa mstakabali wa Taifa letu, hivyo nendeni mkatekeleze jukumu hilo kwa uadilifu”, ameeleza Mwl. Marwa.
Vile vile amewataka washiriki hao kuwa nadhifu, kutumia lugha za staha na kutoa kipaumbele kwa wapiga kura wenye mahitaji muhimu watakapofika kituoni ikiwa ni pamoja na kushirikiana na mawakala wa vyama vya siasa waliowekwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha Washiriki wa mafunzo hayo wameapa kiapo cha kutunza siri na kujitoa uanachama wa vyama vya siasa katika kipindi chote cha utekelezaji wa jukumu lao kama watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
“Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura”.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved