Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Red Cross Society-TRCS) kwa kushirikiana na Baraza la Vijana Mkoa wa Kagera kila mwaka hufanya kambi ya vijana yenye lengo la kuwapa fursa ya kupata elimu na maarifa mbalimbali ya maisha ambayo ni ujasiriamali, ubinadamu na kujitolea katika jamii.
Akifungua kambi hiyo kwa mwaka 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa wilaya ya kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka vijana hao kuzingatia maadili ya kiafrika pamoja na kuwa wazalendo wa nchi zao.
"Tunapofanya kazi zetu tuzingatie maadili ya Kiafrika lakini pia tuzingatie uzalendo wa nchi zetu, hakuna atakayetoka nchi nyingine aje aipende nchi yako hivyo basi uzalendo ndio kipaumbele chetu," amesema Mhe. Msofe
Aidha Mhe. Msofe amewataka vijana kutumia fursa mbalimbali zilizopo, ikiwemo mikopo ya vijana inayotolewa na Halmashauri ili iweze kuwasaidia katika kuwaletea maendeleo na kukuza uchumi wao.

Awali Mwenyekiti wa TRCS Mkoa wa Kagera Ndg. Leonard akieleza lengo la kambi hiyo amesema sio kuwafundisha vijana kupambana na majanga tu bali ni kuwafundisha namna ya kupambana na umasikini kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi ili watakapotoka wakaanzishe vikundi vya wajasiriamali vitakavyo wasaidia kujikwamua kiuchumi.
Kwa mwaka 2025 Kambi hiyo inafanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mabira Wilaya ya Kyerwa kuanzia tarehe 28 hadi 30 Disemba 2025 ambapo jumla ya vijana 500 wa Mkoa wa Kagera na vijana waalikwa kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Burundi, Rwanda,Uganda, Kenya, na Sudan kusini wameshiriki katika kambi hiyo.

Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Copyright ©2025, ICT Department Kyerwa District Council . All rights reserved.