Baraza la Biashara la Wilaya ya Kyerwa limefanya kikao leo tar. 1 Agosti 2023 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa kwa wadau mbalimbali wa biashara kutoka sekta za umma na binafsi kwa lengo la kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.
Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewapongeza wadau wa biashara waliojitokeza na kuwataka kuchangamkia fursa zilizopo ambazo zinaweza kusaidia kukuza uchumi wa Wilaya ya Kyerwa na kuzingatia sharia za biashara ambazo zimewekwa ili kuepusha migongano na serikali.
“Ninaona Kyerwa kuna fursa za kutosha lakini hazitumiki ipasavyo, kuna fursa za kuwepo kwa hifadhi za TANAPA, mazao ya kilimo, ufagaji, kuchimba mabwawa ya samaki, kuchakata mazao na kuacha kuuza ‘raw material’ (malighafi).” ameeleza Mhe. Msofe.
Kwa upande wake Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi za Tanzania (TANAPA), kwa hifadhi za Ibanda na Rumanyika Bw. Charles Ngendo amewataka wafanyabiashara kuwekeza katika hifadhi hizo kwa kuchangamkia fursa za kuchimba mabwawa ya ufugaji wa samaki, miradi ya ufugaji nyuki, kujenga hoteli za kulala watalii, na kutoa huduma za usafirishaji.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kyerwa SACF. James John awaasa wafanyabiashara kuchangamkia fursa za kuwekeza katika hifadhi za Ibanda na Rumanyika ambazo kwa miaka ijayo zitakuwa vivutio vikubwa vya utalii na kuwanufaisha wafanyabishara na Wilaya ya Kyerwa kwa ujumla.
Pia Afisa Biashara wa Wilaya ya Kyerwa Bw. Mathew Rufunjo amewakumbusha wafanyabiashara kuhakikisha wanasajili biashara zao kupitia mfumo mpya wa Tausi ambao unawarahisishia kupata leseni za biashara kwa njia ya kidigitali.
Baraza la biashara Kyerwa hujumuisha taasisi za serikali na wadau kutoka sekta binafsi wakiwemo viongozi na wawakilishi wa wafanyabiashara, pamoja na wadau wa maendeleo.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved