Jumla ya vijana 58 wakike wakiwa 2 na wakiume 56 wamehitimu mafunzo ya jeshi la akiba maarufu kama mgambo ambao waliweka kambi katika Kata ya Kikukuru Wilaya ya Kyerwa tangu Julai 20, 2023.
Akizungumza katika sherehe ya kufunga mafunzo hayo leo Novemba 28, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka vijana hao kuwa waadilifu na wazalendo kwa nchi yao pamoja na kuyatumia mafunzo waliyoyapata kwa maslahi yao na nchi nzima kwa ujumla.
“Tunatumaini kwamba mtatusaidia vyema katika kupunguza uhalifu. Tunategemea kwamba mtaungana na wenzenu ambao walishapata mafunzo na kwa kusaidiana na majeshi mengine ili kusaidia Wilaya ya Kyerwa ibaki salama, amani na utulivu. Kwa mafunzo mliopewa tunaamini kwamba sasa Kyerwa inaenda kuwa na utulivu.” Amesema Msofe.
Aidha kutokana sababu ya baadhi ya vijana kushindwa kujiunga na mafunzo hayo kwa kukosa kigezo cha kuwa na elimu ya msingi. Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa jamii kuwaandikisha watoto wao shule za msingi na wale wanaofaulu kuendelea na sekondari waandikishwe ili watoto wao wasijekukosa fursa mbalimbali hapo baadae.
Kwa upande wake Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Kyerwa SSGT Deomedes Rupia amesema kuwa wahitimu hao wamehitimu mafunzo kwa kiwango kinachotakiwa na watakuwa tayari muda wote kulitumikia taifa lao.
Katika risala yao wahitimu wa mafunzo ya jeshi la akiba wamesema wamejengwa kikakamavu katika kujilinda wao wenyewe, raia na mali zao ikiwa ni pamoja na mafunzo ya matumizi ya silaha, ujanja wa porini, usomaji wa ramani, sheria za mgambo, kwata mbalimbali, elimu ya uraia, kuzuia na kupambana na rushwa, zima moto na mafunzo ya ujasiriamali.
Aidha wamesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza uhalifu katika jamii kwa kudhibiti wizi wa mazao, uvunjaji wa maduka na kupambana na magendo ya kahawa.
Naye DevothaTumainel, miongoni mwa wahitimu wa mafunzo hayo, ameipongeza na kuishukuru serikali kwa kupata mafunzo hayo na kuiomba serikali kuwapa kipaumbele cha kuwapa nafasi za kazi vijana wa kike wanaohitimu mafunzo hayo ili kuwavutia wengine kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa awamu ijayo.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved