Zahanati ya Katera iliyopo katika Kijiji cha Katera Kata ya Isingiro Wilaya ya Kyerwa ambayo ilianza kujengwa toka mwaka 2019 imezinduliwa na kuanza kutoa huduma rasmi tarehe 16 Julai 2024.
Zahanati hiyo iliyogharimu kiasi cha shilingi 153,696,000 ambazo ni fedha kutoka kutoka serikali kuu, mapato ya ndani ya Halmashauri, mfuko wa jimbo pamoja na nguvu za wananchi inatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 3,800 wa Kijiji cha Katera na maeneo jirani.
Akizindua Zahanati hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewashukuru wananchi pamoja na wadau waliochangia ujenzi wa zahanati hiyo hadi kukamilika na kuwataka wananchi wa eneo hilo kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kuwahudumia wananchi.
“Niwapongeze sana wananchi wa Katera kwa kuja na wazo la ujenzi wa Zahanati na kisha mkachangia Sh. 68,201,000 na kutoa nguvu zenu na muda wenu, pia niwapongeze Halmashauri pamoja na kuishukuru Serikali ya awamu Sita Chini Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh. 50,000,000 za umaliziaji wa Zahanati hii” ameeleza Mhe. Msofe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Wilaya ya Kyerwa SACF. James John amewataka wananchi kuendelea kuibua na kuchangia katika miradi ya maendeleo kwani bado kuna unahitaji wa miundombinu ya ujenzi wa nyumba za watumishi pamoja na uzio katika Zahanati hiyo.
Hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa imetenga Sh. 70,000,000 katika mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu mingine iliyobakia katika Zahanati hiyo.
Pia Bi. Yusida Fedelis mwananchi wa Kijiji cha Katera ameishuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajengea Zahanati hiyo ambayo imewapunguzia umbali mrefu wa kufuata huduma za afya katika vijiji vingine.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved