Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa Bw. Mussa Gumbo ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Kyerwa kutunza ubora wa kahawa ili kuepuka kushuka kwa bei katika misimu ijayo na kuendelea kuwanufaisha wananchi, Wilaya na Taifa kwa ujumla.
Bw. Gumbo ametoa wito huo wakati akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika katika Kata ya Isingiro Julai 15, 2025.
“Kahawa hizi zinazozalishwa hapa zinaenda mpaka kwenye soko la kimataifa, tunapoharibu ubora wa kahawa yetu tunajiharibia wenyewe, kwa hiyo nitoe wito kwamba tuendelee kuhakikisha kahawa yetu inakuwa bora na kuitangaza Wilaya ya Kyerwa na Tanzania kwa ujumla,” ameeleza Bw. Gumbo.
Awali Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Meshack Libent akitolea ufafanuzi kuhusu kushuka kwa bei ya kahawa katika Wilaya ya Kyerwa, alieleza kuwa moja ya sababu ni kahawa kukosa ubora na hivyo kuwataka wakulima kuzingatia ubora wakati wa kuvuna, kuanika na kuhifadhi kahawa zao.
“Tuzingatie ubora wa kahawa, tuvune kahawa iliyokomaa vizuri, iliyoiva vizuri, tuikaushe vizuri na tuihifadhi vizuri ili tuweze kupata bei nzuri,” amesema Bw. Libent.
Aidha Katibu Tawala amewataka wananchi kuendelea kusimamia na kutunza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili iendelee kuwanufaisha wananchi wanayoitumia miradi hiyo.
“Kuna wananchi hapa wamehoji juu ya ubora wa makaravati, Niwapongeze sana, haiwezekani mwananchi unaona kitu kimeharibika au hukielewi elewi alafu unakaa kimya, wakati mwingine usisubiri mkutano piga simu moja kwa moja kwa wahusika au viongozi wako ili hatua zichukuliwe,” amesema Katibu Tawala.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved