Mkutano wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa umefanyika leo tarehe 14 Mei 2025 kwa ajili ya kujadili taarifa ya utekelezaji wa robo ya tatu ya kuanzia mwezi Januari hadi Machi kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa Bw. Mussa Gumbo ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa baraza hilo na alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya, ametoa rai kwa Wanakyerwa kukemea kitendo cha wizi wa kahawa unaoendelea katika baadhi ya maeneo huku akiwataka Waheshimiwa Madiwani kushirikiana kupambana na magendo ya kahawa katika kipindi hiki ambacho kahawa imeanza kutoroshwa na kupelekwa nchi jirani.
“Tunao baadhi ya Waheshimiwa Madiwani ambao wanatupa ushirikiano tunawashukuru sana. Lakini tunaomba wengine mtupe ushirikiano. Swala la udhibiti wa magendo ya kahawa sio la mtu mmoja, sio la Mhe. Mkuu wa Wilaya, sio la Mwenyekiti wa Halmashauri na wala sio la Mkurugenzi, ni swala la Wananchi wote kwa hiyo tushirikiane”. Amesisitiza Bw. Gumbo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico ametoa rai ya kubadilishwa kwa mgawanyo wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya 60% inayotumika katika uendeshaji na 40% kupelekwa katika miradi ya maendeleo na badala yake iwe kinyume chake ili kuboresha huduma za jamii katika Wilaya ya Kyerwa.
Aidha amesema Halmashauri imeimarika katika ukusanyaji wa mapato kutoka 1.2 Bilioni hadi sasa ukusanyaji umefikia 6.1 Bilioni katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa baraza lililopo sasa ambalo limepelekea miradi mingi kutekelezwa kwa mapato ya ndani ya halmshauri.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved