Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka wadau wa kahawa kushirikiana kwa pamoja ili kudhibiti biashara ya magendo ya kahawa ambayo huipotezea Serikali mapato.
Ameyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa 37 wa Chama cha Ushirika cha Wilaya za Karagwe na Kyerwa KDCU LMT uliofanyika tar. 5 Aprili 2024 katika ukumbi wa Rweru Wilayani Kyerwa.
“Suala la kudhibiti magendo, suala la kudhibiti kahawa yetu isitoke nje ya nchi si suala la Mkururegenzi peke yake, hili ni suala la wadau wote wa kahawa kwani wote tunafaidika na kahawa hiyo, wote tuna nia njema na nchi yetu na tunatamani pato hili libaki nchini kwetu.
“Kwa hiyo nitoe wito, pale msimu unapokuwa umechanganya, tunapohitaji kuongezewa nguvu basi tuwe tayari kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha tunaweza kudhibiti zao hili.” Ameeleza Mhe. Msofe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Laiser amewata viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) kuwa waaminifu na waadilifu kwa kuhakikisha wanapokea kahawa yenye vigezo ili kuweza kuwanufaisha.
“Inawezekanaje kahawa ikose ubora kama Karani anayesimamia zao la kahawa katika eneo lake amekubali kusimamia haki? Inawezekanaje kwenye vyama vya msingi kuwe na kahawa mbichi?” aliuliza Mhe. Leiser.
Naye Meneja wa Bodi ya Kahawa Mkoa wa Kagera Bw. Edmond Zani ametumia mkutano huo kuwatangazia wadau wa kahawa kuwa msimu mpya wa kahawa unatarajiwa kuanza Mei Mosi mwaka huu.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved