Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka Wananchi kuulinda Muungano wa Tanzania ili umoja na mshikamano baina ya Watanzania uendelee kudumu kwa maslahi ya mapana ya Taifa.
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Aprili 2025 katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano yaliyoambatana na zoezi la kufanya usafi wa mazingira, kupanda miti na kukagua miradi ya vyumba viwili vya madarasa na matundu 24 ya vyoo ambayo imekamilika katika shule ya Msingi Rwensinga iliyoko Kata ya Rutunguru Wilaya ya Kyerwa.
"Watanzania tuko wengi sana lakini niwaambie zaidi ya asilimia 90, tumezaliwa ndani ya Muungano, tuendelee kufundishana na kuwafundisha watoto wetu ili waujue na kuuenzi Muungano wetu", amesema Mhe. Msofe
Mkuu wa Wilaya ametumia Mkutano huo pia kuwakumbusha Wananchi kuhusu Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba Mwaka huu, Huku akiwataka wale ambao hawajahuisha taarifa zao, kushiriki katika zoezi la uboreshaji taarifa kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 1 hadi 7 Mei 2025 katika Wilaya ya Kyerwa.
Vile vile Mhe. Msofe amewataka Wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuleta fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Kyerwa.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni “Muungano wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa, Shiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.”
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved