Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amezindua zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo leo Julai 24, 2025 katika Mnada wa Katera Kata ya Isingiro ambalo ni mpango wa Serikali kutoa ruzuku nchi nzima.
Akiongea na wafugaji waliofika katika eneo hilo, Mhe. Msofe amewahimiza wafugaji wote wa Wilaya ya Kyerwa kuhakikisha wanachanja mifugo yao ili kuongeza ubora na thamani ya mifugo yao katika soko la ndani na nje ya nchi.
“Katika harakati za kuwainua wafugaji Serikali imekuwa na dhamana ya kutafuta masoko nje ya nchi, lakini tukumbuke kwamba kule nje wenzetu wanathamini sana ubora, hatuwezi kupeleka mifugo wala tukapeleka nyama ambazo zimetokana na mifugo dhaifu. Kwa hiyo ni lazima tuzingatie afya ya mifugo.
“Ili kulitekeleza hili, Serikali imeamua kutoa ruzuku kwa wafugaji, tumekuja na huu mpango tuwaombe muupokee kwa nia njema ili kuongeza ubora na thamani ya mifugo yetu,” ameeleza Mhe. Msofe.
Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Kyerwa Dkt. Hassan Msoke amesema jumla ya dozi laki tano ya chanjo ya Ng’ombe 93,984 wanatarajiwa kuchanjwa na kutambuliwa pamoja na wanyama jamii ya ndege, kuku 286,746, bata 32,462, kanga 2,237 na bata mzinga 209. Huku akisema kalenda ya utekelezaji wa zoezi hilo katika Vijiji vyote itaanza rasmi tarehe 4 Agosti 2025 baada ya zoezi la uzinduzi.
Vile vile amesema gharama za kuchanja ngo’mbe mmoja itakuwa shilingi 500, ambayo sawa na nusu ya gharama za kawaida, huku hereni za utambuzi pamoja na chanjo ya wanyama jamii ya ndege zitatolewa bure.
Naye Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Kyerwa Bw. Cleophace Mtungirei ameishukiuru Serikali kwa kuwapelekea ruzuku ya chanjo ya ng’ombe kwa gharama ndogo na kutoa rai kwa wafugaji wote kupeleka mifugo yote ikapatiwe chanjo na kuacha tabia ya kuficha baadhi ya mifugo ili mifugo yote ya Wilaya ya Kyerwa iweze kupatiwa chanjo ikiwa ni pamoja na kufuata maelekezo ya wataalam wa mifugo.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved