Mkutano wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa umefanyika leo tarehe 28 Februari 2025 kwa ajili ya kujadili taarifa ya utekelezaji wa robo ya pili, kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba 2024/2025 katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Rwenkorongo kata ya Kyerwa.
Akiongoza Mkutano huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico amesisitiza Waheshimiwa Madiwani kushirikiana na wataalam wa Halmashauri kuhakikisha uandikishaji wa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waweze kuripoti na kujiunga katika shule walizopangiwa.
Hayo yamejiri baada ya kuwasilishwa taarifa ya hali ya kuripoti kwa wanafunzi na kuonekana baadhi ya shule kiwango cha kuripoti kipo chini huku Shule ya Sekondari Murongo ikiwa na 53% ya wanafunzi walioripoti hadi sasa.
“Huu mkakati wa watoto kwenda shule Waheshimiwa wajumbe kule tuko sisi viongozi wa Kata, twendeni sisi Madiwani tukahamasishe wananchi, watoto wote waende shule. Tukiacha maana yake tunazalisha shida.
“Baraza linaazimia, ikifika tarehe 15 Machi 2025 wanafunzi wote wawe wameripoti shule, Mkurugenzi waandikie walimu barua wape taarifa, watoto ambao hawajaripoti wanawajua kama kuna walioenda shule binafsi wajulikane, tuwaambie wananchi na wazazi wote wa Kyerwa kama mzazi au Mlezi hajampeleka mtoto shule hatua za kisheria zitachuliwa.” Amesema Mhe. Henerico.
Vile vile Mhe. Henerico ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Kyerwa ikiwa ni pamoja na miradi ya afya, elimu, maji, barabara na umeme.
Aidha baraza limepatiwa taarifa ya uwepo wa timu ya wataalam ambayo inapita katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kyerwa kwa ajili ya kutoa elimu ya kudhibiti magonjwa ya kahawa ambayo yanavamia mibuni kwa kasi na kuhatarisha uzalishaji wa zao hilo kuu katika Wilaya ya Kyerwa na kuwataka Wahe. Madiwani na wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam hao.
Pia baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wakichangia katika baraza hilo wameelezea juu ya uwepo wa changamoto ya maji katika kata zao na kuomba zishughulikiwe ili kuwakwamua wananchi wa maeneo yao suala ambalo limechukuliwa na wahusika kwa ajili ya utekelezaji.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved