Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Milambi kilichopo Kata ya Nyaruzumbura kulinda miundombinu ya barabara iliyopo katika maeneo yao ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Amesema hayo katika ziara yake leo Tarehe 22 Februari 2024 katika Kata ya Nyaruzumbura yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi baada ya kupokea taarifa kuwa kuna baadhi ya wananchi huvunja mawe kwenye daraja na kuyatumia katika kufungia nyavu za kuvulia samaki.
“Serikali inatengeneza madaraja. Sasa hizo hela tulizotoa badala ya kusema tuwaletee maji nyie mnataka tupeleke tena kutengeneza daraja ambalo lilishatengenezwa. Sijui mnaona hiyo athari yake?” Aliuliza Mhe. Mkuu wa Wilaya.
“Mwenyekiti wa Kijiji cha Milambi simamia hili. Hayo mawe yakiisha msije mkaanza tena kudai. Wewe unadhamana ya kulinda Kijiji chako, hilo libebe kaa na Wenyeviti wa Vitongoji vyako hususani eneo ambalo hilo daraja lipo muone namna gani ya kulinda pale.” Ameelekeza Mhe. Msofe.
Aidha amewataka wananchi kuwaripoti wahamiaji haramu katika ngazi husika ili wafuate taratibu za kiuhamiaji na waweze kupewa vibali vya muda wa kuishi na kufanya kazi nchini.
Pia kero ya Vitambulisho vya taifa, mkuu wa Wilaya amesema watumishi wa NIDA wataanza kupita Kata kwa Kata ili kuandikisha wananchi ambao hawana vitambulisho na kuwataka wananchi kuandaa taarifa na nyaraka zinazohitajika ili kurahisisha zoezi hilo.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved