MKUU wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe leo tar. 03 Agasti 2023 amehutubia baraza la Madiwani katika kikao cha robo ya nne ya baraza hilo kilichofanyika katika ukumbi wa Rweru Plaza Wilaya ya Kyerwa.
Akizungumza katika baraza hilo Mhe, Msofe amewapongeza Waheshimiwa Madiwani na Watumishi wa Halmashauri kwa kukusanya mapato na kuvuka lengo hadi kufikia asilimia 149 za makadirio ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 na kuwataka kuongeza juhudi katika ukusanyaji na kuibua vyanzo vingine vya mapato katika Wilaya ya Kyerwa.
Vile vile amewataka Waheshimiwa Madiwani wasimamie mapato kwa uadilifu na kuwakumbusha wajibu wa kusimamia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao kwa kuwa wao wanajukumu la kukagua na kusimamia miradi hiyo ili isihujumiwe.
Aidha amewataka waheshimiwa madiwani kuendelea kusisitiza suala la lishe katika kata zao ili kuondokana na utapiamlo unayoisumbua jamii ya Kyerwa. Huku akisisitiza utunzaji wa mazingira katika jamii, hasa kuzuia uchomaji wa moto unaondelea kufanyika katika maeneo mbalimbali na kuvitaka vyombo vinavyohusika kuwachukulia hatua stahiki wale ambao wanafanya uharibifu huo.
Awali akitoa hotuba yake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico amesema Wilaya ya Kyerwa iliidhinishiwa kutumia kiasi cha Sh 39,404,217,740.00 kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za halmashauri zikiwemo kulipa mishahara, matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo ambacho kiasi hicho kimetumika kwa asilimia 100.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kyerwa Mhe. Innocent Bilakwate amewapongeza; Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji na watumishi wa halmashauri, vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi za serikali kwa kushirikana na Waheshimiwa Madiwani kwa kupambana na magendo ya kahawa iliyokuwa ikitoroshwa na kupelekwa nchi za nje na kupelekea kukuza pato la wilaya ya Kyerwa na kuahidi kuendelea kushiriana nao.
Aidha wataalamu kutoka idara mbalimbali za Halmashauri, RUWASA na TARURA waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi na shughuli zao kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambazo zilipokelewa na baraza hilo la madiwani katika wilaya ya Kyerwa.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved