Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amefanya kikao na Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Maafisa Elimu Kata na Walimu Wakuu kujadili swala la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali, darasa la kwanza na waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule zote zilizopo Wilaya ya Kyerwa.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa leo Tar. 26 Januari 2024, Mhe. Msofe amesema ifikapo Tarehe 30 Januari 2024 Walimu Wakuu wapeleke taarifa za uandikishaji kwa Watendaji wa Kata na ikifika Februari 03, 2024 hatua kali za kisheria zianze kuchukuliwa kwa wazazi au walezi ambao hawatawandikisha watoto wao.
Awali akitoa taarifa ya hali ya uandikishaji katika Wilaya ya Kyerwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Afisa Elimu Sekondari Mwl. Stephano Ndabazi amesema mpaka sasa Wilaya ya Kyerwa imeandikisha wanafunzi wa awali 73.7%, darasa la kwanza 82.7% na Kidato cha kwanza 61.5%. na uandikishaji unaendelea.
Mkurugenzi Mtendaji Ameongeza kuwa, Serikali imetoa kiasi cha Tshs. 1,558,100,000 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika shule za sekondari ambazo ujenzi wake utaanza hivi karibuni ili miundombinu hiyo iweze kutosheleza mahitaji ya wanafunzi wote pamoja na wanaoandikishwa.
Aidha baada ya kupokea taarifa ya mapokezi ya fedha, Mkuu wa Wilaya Mhe. Zaituni Msofe amewataka Watendaji na Wakuu wa Shule kusimamia miradi kwa uadilifu na kujenga miradi iliyo bora na kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kusimamia suala hilo kwa ukaribu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico amewataka Watendaji wa Kata kuwajibika kwa nafasi zao kwa kuwatangazia wananchi kwa kuandaa matangazo na kupita kijiji kwa kijiji na Kitongoji kwa Kitongoji ili kuhamasisha wazazi na walezi kuwaandisha watoto wao.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved