Wadau wa Kahawa wamekutana leo tar. 04 Januari 2024 katika ukumbi wa Rweru Plaza kujadili namna ya kukuza uzalishaji wa zao la kahawa katika Wilaya ya Kyerwa.
Akiongoza kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka wadau wenye uwezo kuwekeza katika Wilaya ya Kyerwa na kuongeza thamani ya zao la kahawa kwa kutokutegemea kuuza kahawa ya maganda tu.
Aidha ametoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na Maafisa Ugani kuendelea kufanya ufuatiliaji na usimamizi kwa wakulima wa zao la kahawa kuanzia kitaluni hadi wanapofika hatua ya kuvuna mazao yao na sio kusubiri msimu wa mavuno ndio wanaanza kufuatilia uuzaji wa zao hilo.
Vile vile ameitaka bodi ya kahawa kuongeza uzalishaji wa miche ya kahawa katika Wilaya ya Kyerwa kwani ni Wilaya inayoongoza uzalishaji wa zao hilo katika Mkoa wa Kagera na miche inayozalishwa kwa sasa haikidhi mahitaji ya wakulima wa Wilaya ya Kyerwa.
Aidha amewapongeza wadau wote waliopambana na kuzuia magendo ya kahawa iliyokuwa inatoroshwa na kuvushwa kwenda nchi jirani na pia ile iliyokuwa inavushwa kwenda Wilaya nyingine na kupelekea Wilaya ya Kyerwa kukosa mapato.
“Tulipambana kuona kahawa ya Kyerwa inahesabika Kyerwa na kuhakikisha ushuru unaingia katika Halmashauri yetu ya Kyerwa. Niwashukuru wale wote tulioshirikiana kudhibiti na tutaendelea kudhibiti kuhakikisha kwamba tunapata tunachokistahili kama wazalishaji wa kahawa.” Amesema Msofe.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kyerwa Mhe. Innocent Bilakwate amewataka wataalamu kufanya utafiti wa magonjwa ya kahawa. “Kung’oa na Kuchoma kahawa ndio kuua wadudu? fanya utafiti, tuletee dawa tukaue wadudu wale wanaoharibu kahawa.” Alisema Mbunge.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico amewataka KDCU na vyama vya msingi kununua kahawa ya Ndagashe ambayo ipo kwa kipindi hiki kwani muda unakwenda na kuacha kusubiri kahawa ya msimu tu.
Akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya zao la Kahawa kwa wadau wa kahawa Wilaya ya Kyerwa, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Meshack Libent amesema Wilaya ya Kyerwa kwa mwaka 2023/2024 imegawa Miche 2,722,282 na mwaka 2024/2025 inatarajia kugawa miche 3,500,000.
Aidha katika mavuno ya kahawa katika Wilaya ya Kyerwa kwa mwaka huu 2023/2024 ambao bado unaendelea tayari Wilaya imevuna tani 30,302 na makisio ya mwaka 2024/2025 yanatarijiwa kuwa tani 40,000.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved