Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe leo tarehe 2 Oktoba 2023 amezindua zoezi la ugawaji wa miche ya kahawa kwa wakulima katika Kijiji cha Karenge Kata Isingiro Wilaya ya Kyerwa.
Katika uzinduzi huo Mhe. Mkuu wa Wilaya amewataka wakulima kuwa wazalendo na kwenda kuipanda katika mashamba yao na kuwaonya wale ambao wanania ya kwenda kuuza miche hiyo kwa watu wengine au nje ya nchi.
“Serikali inagawa miche hii kwa wakulima lengo si kwenda kuuza, unapopewa miche hii naamini unaeneo la kwenda kupanda lakini kama haitoshi wapo watu ambao huchukua hatua ya kwenda kuuza miche hii, nitamke wazi kwamba atakapobainika mtu tusilaumiane. Kwa hilo serikali haina masihara.
Tunawapenda wananchi wetu, tunapenda mkuze vipato, mbadilishe maisha yawe mazuri na huduma inayotolewa hapa ni kwa Watanzania na si vinginevyo, kama unategemea kwenda kuuza acha kwa sababu tutafuatilia” ameeleza Mhe. Msofe.
Awali akitoa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kyerwa iliyosomwa na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Meshack Libent amesema Wilaya ya Kyerwa imeotesha Miche 1,766,500 ambayo inatarajiwa kugawiwa kwa wakulima wa Wilaya ya Kyerwa Mwaka huu.
Aidha amesema wakulima watakaopatiwa miche hiyo ni wale waliojiandikisha kwa viongozi wa Kata au AMCOS zao na Mkulima atatakiwa kwenda na fomu iliyosainiwa na viongozi hao ili aweze kupatiwa miche na zoezi hili litaendelea hadi tar. 16/10/2023.
Vile vile ameeleza kuwa Wilaya imekusanya tani 38,652 za kahawa mwaka 2022/2023 na bado makusanyo yanaendelea na imejiwekea mikakati ya kukusanya tani 45,000 ifikapo 2025 ikiwa ni pamoja na kuendelea kuzalisha miche bora ya Kahawa.
Pia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kyerwa Mhe. Bahati Heneriko ametoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda ili kuongeza thamani ya zao hilo.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved