MKUU wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe leo tar. 6 Julai 2023 amezindua mpango wa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika Kituo cha Afya Nkwenda.
Akizungumza katika hafla hiyo amewahimiza wanchi wa Kyerwa kuchangamkia fursa hiyo ya kuwachukulia watoto wao vyeti vya kuzaliwa kwani vinafaida nyingi kwa mtoto na taifa kwa ujumla ambapo huduma hii inatolewa bure.
“Cheti cha kuzaliwa kina matumizi mengi; Hutumika katika kuandikisha watoto wanaoanza elimu ya msingi na wale wanaojiunga na elimu ya sekondari na sasa hivi huwezi kupata nafasi ya kujiunga elimu ya juu pamoja na kupata mikopo kwa ajili ya masomo hayo bila kuwa na cheti cha kuzaliwa.
Vile vile nyaraka hii ni kiambatanisho cha msingi ili kupata nyaraka nyingine za utambulisho kama kadi ya kupiga kura, kitambulisho cha taifa, pasi ya kusafiria, leseni ya udereva, mifuko ya Bima ya afya. Cheti cha kuzaliwa pia ni muhimu ili kupata ajira katika taasisi mbalimbali. Cheti cha kuzaliwa hutumika kubainisha mahusiano kati ya wanafamilia, vile vile kuisaidia serikali kupata takwimu.” Alisema Msofe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa SACF. James John amesema mpango umeratibiwa vizuri, na halmashauri imejipanga vizuri kutekeleza zoezi hili kwa kuwapatia mafunzo stahiki, wasajili wasaidizi wote na kuna vifaa vya kutosha ambavyo vitasaidia zoezi hili kufanyika kikamilifu.
Pia Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Bahati Henerico amewapongeza wazazi hasa akinamama wa Kyerwa ambao wamejitokeza kwa wingi katika zoezi hili la kuwachukulia watoto wao yeti vya kuzaliwa.
Zoezi hili ambalo litafanyika kwa wiki mbili na baada ya hapo litaendelea kufanyika taratibu ili kuhakikisha kila mtoto anapata cheti cha kuzaliwa na limelenga kuwapatia watoto wapatao 66,745 katika wilaya ya Kyerwa ambalo limeratibiwa RITA.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved