Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewapongeza Viongozi na Wananchi wa Kata ya Bugomora kwa kuweka mpango uliyoonesha tija katika kudhibiti magendo ya kahawa na kuzitaka Kata zingine kuiga mfano huo.
Amesema hayo katika ziara yake ya tarehe 3 Juni 2024 ikiwa na lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi zinazowakabili katika maisha yao na kuhitaji ufumbuzi kutoka serikalini.
Mhe. Msofe amefurahishwa na mpango uliowekwa na kamati ya maendeleo ya Kata hiyo kwa kuitisha mikutano ya wananchi na kuwaeleza juu ya udhibiti wa magendo ya kahawa, kuweka vizuizi katika barabara zote za Kata hiyo zinazoelekea mwaloni na kuazimia kwa pamoja kuwa hawatashirikiana na yeyote atakayekamatwa na wadhibiti wa kahawa akiwa anatorosha kwenda nchi jirani.
“Mdhibiti namba moja ni wewe Mwananchi, nyinyi mnafahamiana nani anavusha, nani anapeleka Chama cha Msingi, nani anavuna kahawa mbichi, nani anahusika kwenye wizi wa kahawa. Niwaombe sana ushirikiano wenu na niwashukuru sana wale ambao tumekuwa tukishirikiana nao kwa njia ya simu, kupeana taarifa ili kuweza kudhibiti utoroshaji wa kahawa nje ya nchi yetu,” Ameeleza Mhe. Msofe.
Awali akieleza mpango huo Diwani wa Kata ya Bugomora Mhe. Batinoluho Kamala amesema mpaka sasa wamekamatwa watoroshaji wanne katika Kata hiyo na wametozwa faini huku akimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa wamejipanga kupambana na magendo na tayari AMCOS zao zimeanza kupokea kahawa ya msimu huu.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved