Wilaya ya Kyerwa imeadhimisha miaka 62 ya Uhuru kwa kufanya Mdahalo maalumu uliowakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kupeana elimu ya mambo yaliyofanywa na Serikali pamoja na kukumbushana historia ya Wilaya hiyo tangu uhuru wa Tanzania Bara Disemba 9, 1961.
Akizungumza baada ya mdahalo huo Mwenyekiti wa Maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewashukuru wadau waliojitokea na kuchangia maoni yao katika mdahalo huo ambao umemsadia kuijua Kyerwa ilikotoka, ilipo na kutafuta namna ya kuipeleka mbele.
Aidha amewataka Wanakyerwa kuishi na kauli mbiu ya maadhimisho ya Uhuru ya Mwaka huu isemayo Umoja na Mshikamano ni Chachu ya Maendeleo ya Taifa Letu. Mhe. Msofe amesema, “Hakika bila kuwa na umoja hatuwezi kupiga hatua … tuendelee na ‘spirit’ tulionayo ya kuwa wamoja na tushikamane kweli kweli katika kuleta maendeleo ya Wilaya yetu.”
Akiongoza Mdahalo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa SACF. James John amesema Wilaya ya Kyerwa imepiga hatua katika Nyanja mbalimbali za maendeleo ya Uchumi na uzalishaji ikiwemo; Kilimo, Mifugo, Uvuvi, barabara, umeme, na huduma za kijamii kama Maji, Elimu na Afya ukilinganisha na miaka michache iliyopita.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico amependekeza kuwe siku ya Kyerwa (Kyerwa Day) ambayo itawakutanisha wadau na wananchi ili kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoihusu Wilaya ya Kyerwa jambo ambalo limeungwa mkono na Mkuu wa Wilaya na litatafutiwa siku maalumu.
Naye katibu wa Wazee Wilaya ya Kyerwa Mzee Ezekia Kanyonyi ameeleza historia ya Kyerwa na Mkoa Kagera kwa ujumla na kuwaomba Watanzania wamkumbuke na Kumuombea Mwl. Julius Nyerere ambaye alipigania Uhuru wa Taifa hili. Huku akizungumzia historia ya maendeleo ya elimu na miundombinu ya barabara ambayo kwa sasa imepiga hatua kubwa kwani zamani walitumia siku tatu kusafiri kutoka Kyerwa Mpaka Bukoba.
Baada ya Mdahalo huo Mhe. Msofe ameongoza zoezi la upandaji wa miti ya matunda katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa.
Mdahalo huo ulihudhuriwa pia na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Katibu Tawala wa Wilaya, Wakuu wa Taasisi za Umma, Mhe. Diwani wa kata ya Kyerwa, Wazee maarufu, watumishi na Wananchi wa Wilaya ya Kyerwa na umefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved