Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti imetembelea maeneo mbalimbali ya mto Kagera Wilayani Kyerwa ambayo yanatumika katika biashara ya Magendo ya Kahawa na bidhaa nyingine. Katika Ziara hiyo Wilayani Kyerwa Kamati hiyo iliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Rashid M. Mwaimu. Aidha katika Ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amefanya vikao vya ndani na viongozi na pia Mikutano na wananchi wa vijiji vya Kijumbura na Rwabikagate. Katika Ziara hiyo alitoa pia fursa kwa wananchi kueleza changamoto na sababu zinapelekea biashara hiyo kushamiri katika maeneo yao. Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea kueleza nia ya Serikali ya Awamu ya tano katika kuwahudumia wananchi na kuwaasa kukomesha biashara hiyo isiyokubalika "Hakuna sababu yoyote inayoweza kufanya kukubalika kwa biashara hiyo haramu kwa namna yoyote ile, Nitaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote wanaojihusisha na biashara ya Magendo" alisema Mkuu huyo wa Mkoa kwa msisitizo.
Mkuu wa Mkoa alihitimisha Ziara yake hiyo maalumu kwa kuagiza wale wote wanajihusisha na biashara ya Magendo kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kuagiza uongozi wa Wilaya kuendelea kutoa msaada pale inapohitajika kwa viongozi wanaopambana na biashara ya Magendo ya Kahawa kwenda nchi jirani. Aidha ameagiza kuwa kama kuna wafanya biashara wanaonunua Kahawa kwa bei ya kuridhisha nchi jirani ya Uganda wafike katika mamlaka husika ili wafuate taratibu zinazotakiwa waweze kununua Kahawa hiyo kwa utaratibu unaotakiwa kuliko kuendelea kufanya kwa njia zisizokubalika.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved