Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Mussa Gumbo leo 1 Septemba 2023 ameshiriki katika hafla ya kuwapongeza Walimu wa Shule ya Sekondari Mabira iliyoandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kwa ajili ya kuwapongeza na kuwapa motisha walimu wa shule hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mhe. Gumbo amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa kufaulisha wanafunzi wote na kuupongeza uongozi kwa kuwa na ushirikiano ambao umepelekea ufaulu huo na kushika nafasi ya tatu katika Mkoa wa Kagera kwa shule za serikali.
Aidha amewataka waalimu pamoja na wanafunzi kuendelea kujituma zaidi ili kuendelea kufanya vizuri huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Wanamabira na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji kuipa kipaumbele Shule ya Sekondari ya Mabira kwa kutenga fedha za mapato ya ndani na kutatua changamoto za shule hiyo ikwemo ya mabweni na uzio wa shule hiyo.
“Pamoja na shule kufanya vizuri walimu mnanafasi kubwa katika jamii kwa kuchunga maadili, kwani mnajua wanafunzi wanatoka kule majumbani na kuja shule, niwaombe muendelee kufuatilia mienendo na tabia za wanafunzi wetu,” Amewaasa Mhe. Gumbo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano na serikali na Wataalamu wa Halmashauri kwa kusimamia fedha za miradi ya maendeleo ili iweze kuwanufaisha wananchi wa Kyerwa.
Mhe. Bahati ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka miwili, Wilaya ya Kyerwa tayari imeanzisha shule kumi za kidato cha tano na sita na kuwataka walimu wa shule ya Sekondari Mabira kujitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuwa mfano kwa shule zingine mpya za kidato cha tano na sita katika Wilaya ya Kyerwa.
Akitoa neno la utangulizi Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Mwl. Stephano Ndabazi amesema shule hiyo ambayo imetoa wahitimu wa kidato cha sita kwa mara ya kwanza ilifaulisha wanafunzi wote; kwa daraja la kwanza 42, daraja la pili 26 na daraja la tatu alikuwa mwanafunzi mmoja tu, na shule hiyo changa kushika nafasi ya tatu katika mkoa wa kagera kwa shule za sekondari za serikali.
Katika hafla ya utoaji motisha kwa waalimu waliofaulisha wanafunzi katika mtihani wa taifa, kidato cha sita Mei 2023, katika Shule ya Sekondari Mabira Walimu wote walipewa zawadi, ikiwemo fedha tasmu Pamoja na vyeti ikiwa ni njia mojawapo ya kuwapa motisha wa kuendelea kujituma huku walimu waalikwa wa shule nyingine za Sekondari za Wilaya ya Kyerwa wakitakiwa kuiga na kujifunza kwa kile walichokifanya walimu wa Shule ya Sekondari Mabira.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved