Leo Tar. 28 Septemba 2023 Wazee wa Wilaya ya Kyerwa wameadhimisha Siku ya Wazee Duniani katika Kata ya Nyakatuntu na kutoa matamko kadhaa kwa serikali na jamii yakiwemo ya mmomonyoko wa maadili, wazee kunyang’anywa mali zao, kunyanyaswa kijinsia na mauaji ya vikongwe.
Wazee hao pia wameishauri serikali kujenga Nyumba ya Makumbusho ambayo itatumika kutunza zana na utamaduni wa Wanakyerwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na hata kuvutia watalii katika Wilaya ya Kyerwa.
Akitoa hotuba yake MKuu wa Wilaya ya Kyerwa iliyosomwa na Katibu Tarafa wa Tarafa ya Mabira Bw. Mussa Jumanne amesema serikali itahakikisha inawalinda na kuwathamini Wazee na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za matibabu.
“Tutahakikisha yeyote atakayebainika kumnyanyasa Mzee tunashughulika naye. Hatuwezi kupoteza watu kwa sababu ya ushirikina. Wazee wananyang’anywa ardhi. Mzee bado yuko hai kijana anataka apewe urithi! Ukiona unataka ardhi nenda katafute sehemu nyingine na sio kuwanyang’anya Wazee.” Amesema Bw. Jumanne.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Msafiri Lewanga ambaye pia alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa amewataka wazee kupima afya zao mara kwa mara kwani wao ni rahisi kushambuliwa na maradhi mbalimbali na wakibainika wapatiwe matibabu ili kulinda afya zao.
Maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani hufanyika kila mwaka na kilele chake huwa ni Oktoba Mosi yakiwa na lengo la kuelimisha jamii juu ya haki stahiki zinazohitajika kutolewa kwa wazee wote Duniani. Kauli mbiu ya Mwaka 2023 ni “Uthabiti wa Wazee Kwenye Dunia yenye Mabadiliko”
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved