Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico leo Tar. 15 Machi 2024 amezindua mafunzo ya mfumo wa uwezeshaji wataalam kutambua, kusajili na kutoa vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo ndogo nchini ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Kyerwa.
Zoezi la kutoa mafunzo hayo limewahusisha Watendaji wa Kata zote 24 za Wilaya ya Kyerwa, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Viongozi wa Wafanyabiashara ndogo ndogo pamoja na Viongozi wa Bodaboda wa Wilaya ya Kyerwa yakiwa yamelenga kuwajengea uwezo wa kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi katika maeneo yao.
Akizungumza na washiriki hao Mhe. Henerico amewataka washiriki hao kutambua jukumu lililoko mbele yao kuwa ni kwenda kusimamia na kutekeleza zoezi kwa wafanyabiashara ndogo ndogo katika Kata zao na kufanikisha zoezi hilo ipasavyo kwani linategemea juhudi zeo.
“Kwenye zoezi hili nyinyi ndiyo timu ya ushindi na Serikali inawatazama kwa jicho la kipekee katika kuleta mageuzi yatakayowezesha wafanyabiashara ndogo ndogo wote kwenye Halmashauri yetu kutambuliwa, kusajiliwa na kupatiwa vitambulisho vya kidigitali ili waweze kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.” Ameeleza Mhe. Henerico.
Kwa upande wake Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Bw. Methew Rufunjo ameeleza umuhimu wa zoezi la kuwatambua, kuwasajili na kutoa vitambulisho vya kidigitali kwa wafanyabiashara ndogo ndogo na kuingizwa katika kanzi data ya pamoja na kufungua fursa mbalimbali ikiwemo kupata mikopo yenye masharti nafuu.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku moja kwa wataalam hao na baada ya hapo watatakakiwa kuanza zoezi la kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara katika maeneo yao.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved