Maadhimisho ya siku ya fimbo nyeupe duniani kwa Wilaya ya kyerwa yamefanyika leo tarehe 28 Novemba,2017 katika kata ya Rukulajo.Siku hii ni maalumu ambayo huadhimishwa kote ulimwenguni kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho (hasa wale waliopoteza uoni, yaani wasioona).Fimbo nyeupe, ni fimbo maalumu inayotumika na mtu asiyeona, ilikumtambulisha kwa watumiaji wengine wa barabara , wakati wowote na hasa anapokuwa akitembea.Katika kuadhimisha siku hii mgeni rasmi mheshimiwa Kanali Mstaafu Shaban I.Lisu -Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa alisisitiza wasioona wasinyanyapaliwe katika nyanja zote na aliahidi kutoa fimbo nyeupe moja kwa wasioona.Aidha naye kaimu mkurugenzi wa Halmashauri Mhandisi Juma Magotto aliahidi kutoa jumla ya fimbo nyeupe tatu kwa walemavu wa macho walioshiriki maadhimisho hayo.
Katika sherehe hii,shughuli mbalimbali zilifanyika,ikiwa ni pamoja na kusoma risala ambayo ilisomwa na ndugu Verena Goldian ambaye ni mlemavu wa macho kutoka kata ya Isingiro ambaye alishukuru jinsi Serikali inavyowasaidia kupata fursa za elimu kupitia shule na vyuo maalum kwa watu wasioona kama shule ya sekondari Mabira,shule ya Msingi Kihanga zilizopo hapa Wilayani.Aidha vyuo vya ufundi stadi vya Korogwe na Sengerema vimekua na mchango mkubwa katika kuwanoa walemavu wasioona.Shughuli nyingine zilizofanyika katika kilele hicho ni maigizo ya changamoto na umuhimu wa fursa za kielimu yaliyoonyeshwa na wanafunzi wa shule ya Msingi Nyabikurungo,ushonaji wa nguo na vitambaa yaliyoonyeshwa na mshiriki asiyeona ndugu Verena Goldian.
Lengo la maadhimisho ya siku hii, ni kuihamasisha jamii na watumiaji wote wa barabara kama vile madereva, kuiheshimu fimbo nyeupe na kumsaidia asiyeona anapotembea na anapovuka barabara. Pia siku hii hutumika kutambulisha shughuli mbalimbali zinazofanywa na wasioona, malengo yao, mahitaji yao, uwezo wao katika suala zima la maendeleo, changamoto wanazokabiliana nazo, na mchango unaohitajika toka Serikalini na wadau wengine wa maendeleo.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Mkataba wa Marrakesh uondoe vikwazo vya kusoma kwa wasioona”. Marrakesh ni mji katika nchi ya Morocco ambapo Serikali ya Tanzania iliridhia mkataba wa Kimataifa ili kutatua changamoto zinazowakabili watu wasioona ili nao wawe chachu ya kasi ya maendeleo nchini.Mkataba huu unataka kuchapwa kwa majarida ya nuktanundu au kuwekwa kwa sauti ili kuwasaidia watu wasioona kusoma na kupata taarifa mbalimbali.
Jumla ya washiriki takribani 250 walishiriki katika kilele cha maadhimisho ya siku hii.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved