Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, imezindua zoezi la ugawaji wa miche ya Kahawa 5,161,666 kwa wakulima katika msimu wa mwaka 2025/2026 leo tarehe 17 Oktoba 2025 katika kitongoji cha Karenge Kijiji cha Karukwanzi Kata ya Isingiro.
Akizindua zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mhe. Zaituni Msofe ameipongeza Halmashauri ,Bodi ya Kahawa pamoja na sekta binafsi kwa kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha wanazalisha miche bora ya kahawa itakayo wanufaisha wakulima wa Wilaya ya Kyerwa.
Akizungumza na wakulima waliojitokeza katika zoezi hilo Mhe.Msofe amewataka Maafisa Kilimo kuweka utaratibu wa ufuatiliaji wa wakulima baada ya zoezi la ugawaji wa miche ili kuhakikisha miche hiyo inaleta manufaa kwa wakulima.
“Tuwafikie wakulima tuwashauri vizuri ili sasa miche hii tunayoigawa iende ikatunzwe na iweze kukua hatimaye tupate faida na lengo tulilolikusudia tuweze kulipata” ameeleza Mh. Msofe.
Naye Bw. Meshack Libent, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi amesema kuwa mwaka huu miche imeongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma hivyo kutakuwa na ongezeko la ugawaji wa miche na kutoa rai kwa wakulima kutumia mvua za vuli na kuhakikisha wanapanda miche yao, kwa kuwashirikisha maafisa ugani.
Dr. Albert Katagira, Mkurugenzi wa JJAD, kampuni inayojishughulisha na kilimo cha kahawa amesema miche hiyo ni bora na inachukua muda mfupi kwa kuanza kutoa mazao kwa mwaka mmoja "Miche hii ni bora na ya kisasa, wananchi ni mashahidi, kwa waliochukua mwaka juzi na mwaka jana, wamenufaika.”
Kwa upande wake Bi. Mary Clemence mkulima wa kahawa katika Kata ya Isingiro ameishukuru Serikali pamoja na Halmashauri kwa kuzindua zoezi hilo la ugawaji wa miche bora ya kahawa, kwani kupitia kilimo cha kahawa kimewasaidia wanawake wengi katika kutengeneza Uchumi wao binafsi.
Pia Bw. Tumaini clavery, ameishukru na kuipongeza Serikali kwani kupitia zao la kahawa vijana wengi wameweza kujikwamua kiuchumi.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved