Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapatia wananchi wa Wilaya ya Kyerwa Magari mawili yatakayotumika katika kutolea huduma za afya ambayo ni gari lakubebea wagonjwa (Ambulance) litakalotumiwa katika Kituo cha Afya Murongo pamoja na gari la usimamizi wa shughuli za afya katika Wilaya ya Kyerwa.
Akikabidhi magari hayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa Mhe. Innocent Bilakwate leo Tar. 21 Februari 2024 katika Kituo cha Afya Murongo na kushuhudiwa na wananchi waliojitokeza kujionea zoezi hilo amemshukuru Rais Samia kwa kutoa magari hayo.
Mhe. Mbunge ametoa rai kwamba yatumiwe kwa kazi iliyokusudiwa na akisisitiza juu ya ‘Ambulance’ kubaki katika kituo cha Afya cha Murongo kutokana na eneo hilo kuwa mpakani na kuwa na umbali mrefu hadi kufika katika hospitali ya Wilaya na Maeneo mengine.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe ameishukuru Serikali inayoongozwa na chama cha CCM chini ya Rais Mama Samia kwa kuipatia Wilaya ya Kyerwa Magari hayo pamoja na Mbuge kwa kuisemea na kuipambania Wilaya kwa nafasi yake hadi Kupata Magari hayo.
Vile vile amewataka watumiaji wa magari hayo chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kuyatunza na kuhakikisha yanawasaidia wananchi.
“Ukiona umependelewa umepewa Dhahabu basi itunze, kwa hiyo nitoe rai kwa wale wanaohusika na magari haya, magari haya yatunzwe vizuri, lakini yatumike kwa shughuli iliyokusudiwa na si vinginevyo,” Amesema Mhe. Msofe.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved