Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa imefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo kwa kipindi cha Robo ya tatu ya mwaka 2023/2024.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Bahati Henerico akiambatana na Wajumbe wa kamati hiyo pamoja na Wataalam kutoka Halimashauri ya Wilaya ya Kyerwa wametembelea na kukagua miradi sita ya sekta ya elimu, afya, Biashara na mifugo.
Katika miradi iliyokaguliwa ni pamoja na Shule Mpya ya Sekondari ya Bugara Millennium iliyopo Kata Bugara iliyogharimu kiasi Tsh 558,145,130.50 fedha kutoka Serikali Kuu (SEQUIP) ambayo tayari imepokea wanafunzi na mradi umeanza kutoa huduma kwa jamii.
Aidha kamati ilitembelea ujenzi wa Zahanati ya Businde ambayo ilipokea Tsh 50,000,000 toka Serikali Kuu kwa ajili ya umaliziaji wa zahanati hiyo iliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi toka 2021, ambao walishachanga na kutumia Tsh 47,000,000 na mradi uko katika hatua ya umaliziaji.
Vilevile kamati ilitembelea ujenzi wa miundombinu ya usafi wa mazingira katika Zahanati ya Nyamiaga Kata ya Bugomora ambayo ilipokea fedha kiasi cha Tsh 80,000,000/= kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa kisima cha maji, vyoo, mnara wa tanki, kichomea taka, na kinawia mikono ambayo ujenzi umefikia hatua ya umaliziaji.
Katika Kata hiyo, Kamati pia ilitembelea mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu nane ya vyoo katika shule ya Serondari ya Lut. Gen. Silas Mayunga wenye thamani ya Tsh 114,400,000/= ambapo mradi uko katika hatua ya umaliziaji.
Miradi mingine ni soko la ndizi la Murongo ambapo kamati ilitembelea na kujionea hali ya biashara na usafi wa mazingira katika soko hilo ambalo linasimamiwa na Serikali ya Kijiji na kuwataka watendaji kuimarisha usafi katika eneo hilo na pia Ujenzi wa Machinjio ya Isingiro uliogharimu Tsh 16,000,000/= uliojengwa kwa mapato ya ndani.
Mwenyekiti wa Halmashauri kwa niaba ya kamati aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na kuhimiza ukamilishaji wa miradi kwa wakati huku akiwataka wasimamizi kubana matumizi na kuhakikisha miradi yote inakamilika na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved