Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kyerwa imetembelea na kukagua miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Bilioni tano inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi.
Akiongoza ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ndg. Daniel Damiani amesema ameridhishwa na usimamizi wa miradi ambayo inatekelezwa katika Wilaya ya Kyerwa na kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji na Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa juu ya kumalizia miradi hiyo.
“Miradi yote tuliyoitembelea imesimamiwa kwa ubora, imesimamiwa vizuri na imejengwa kwa viwango na tunaagiza shule za sekondari mbili kufikia mwaka kesho ziwe zimesajiliwa na zianze kupokea wanafunzi na wananchi wajue faida ya kuendelea kuchangia zile sekondari kwa vile zitaondoa msongamano katika shule mama za wilaya yetu.” Alisema Damiani.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kyerwa Mhe. Innocent Bilakwate amempongeza Mkurugenzi Mtendaji pamoja na timu nzima ya halmashauri kwa kudhibiti utoroshaji wa kahawa na kuongeza ukusanyaji wa mapato amabayo yanasaidia kukamilisha miradi kwani kipindi cha nyuma kulikuwa na maboma yaliyotelekezwa na wasimamizi jambo ambalo lilikuwa linarudisha nyuma maendeleo ya wilaya.
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Bahati Henerico amesema halmashauri wamejipanga katika kukusanya na kusimamia mapato na fedha inayopatikana itapelekwa katika miradi ya maendeleo na kuwataka wananchi waendelee kushiriki katika maendeleo ya wilaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa SACF. James John amesema kwa mwaka wa fedha uliopita serikali ilitoa zaidi ya Bilioni 38 kwa matumizi ya kawaida ya miradi ya maendeleo katika wilaya ya Kyerwa, na amepokea maelekezo yote ya chama na yatafanyiwa kazi.
Katika ziara hiyo kamati ya CCM Wilaya ya Kyerwa imetembelea miradi mitano ambayo ni mradi wa hospitali ya wilaya ambao umegharimu kiasi cha shilingi 2,100,000,000/= na ulianza kutoa huduma mwaka 2020, mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA ambao umeanza kutekelezwa Juni 2023 wenye thamani ya Bilioni tatu.
Pia ujenzi wa shule ya msingi mpya ya mwangaza iliyopo kata ya Kikukuru, kijiji cha Mukunyu wenye thamani ya kiasi cha shilingi 540,300,000/=. Mradi wa shule ya sekondari Makazi uliopo kata ya Mabira ambao vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja vimekamilika na vimegharimu shilingi 80,973,881/=
Pamoja na mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Umoja iliyopo kata ya Rwabwere kijiji cha Umoja wenye thamani ya shilingi 44,939,600/= ambao ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa viko katika hatua ya umaliziaji.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved