Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajjat Fatma Mwassa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Mhe. Hajjati Mwassa ametoa pongezi hizo katika baraza maalumu la madiwani ambalo limeketi leo tar. 28 Mei 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na kusema kuwa, Kyerwa inajitahidi kusimamia matumizi ya fedha na kusimamia vizuri miradi ya maendeleo.
Aidha ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kwa ukusanyaji wa mapato na kuvuka lengo la mwaka huku akiitaka menejimenti kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuzidi kukuza pato la Halmashauri na kuendelea kuleta maendeleo zaidi.
Kwa upande mwingine ametangaza neema ya bei ya zao la kahawa ambayo amesema kuwa bei ya kahawa msimu huu itaanzia shilingi 3,763 na minada itaanza mapema wiki ijayo.
Pia amewataka waheshimiwa madiwani kwenda kufanya mikutano ya hadhara na kuwaeleza wananchi kuachana na biashara ya magendo ya kahawa kwani inapelekea nchi kukosa mapato na kunufaisha nchi jirani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amesema ataendelea kutoa ushirikiano kwa Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu wa Halmashauri ili kuendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa fedha na miradi ya serikali na kupata hati safi.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved