Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kyerwa leo Tar. 19 Februari 2024 imepokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020/2025 kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2023 katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Kyerwa.
Taarifa hiyo imewasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe katika kikao hicho ambayo imeeleza juu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na serikali katika Wilaya ya Kyerwa.
Mkuu wa Wilaya ameeleza shughuli za Idara na Vitengo pamoja na taasisi za Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Sekta ya Elimu, Afya, Kilimo na Umwagiliaji, Mifugo na Uvuvi, utawala na utumishi, TEHAMA, ardhi, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Wakala wa Maji, Umeme pamoja na barabara.
Aidha amekishukuru Chama cha Mapinduzi kwa ushirikiano kinachotoa kwa Serikali katika Wilaya ya Kyerwa “Niwashukuru viongozi wangu wa Chama kwa maana ya kwamba tumekuwa tukishirikiana bega kwa bega, pale ambapo kuna changamoto tunaitana tunaelekezana tunasonga mbele. Ushirikiano wa Chama na Serikali ndio yametufikisha hapa tulipo. Niwaombe tuendelee kushirikiana na tuendelee kuchapa kazi” amesema Mhe. Msofe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya Kyerwa Ndg. Daniel Damiani amesema wameridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kumpongeza Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na Taasisi nyingine za Serikali na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuendelea kuijenga Wilaya ya Kyerwa.
Aidha Mwenyekiti huyo amewatunuku vyeti vya utendaji kazi mzuri na kutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Kyerwa kwa Mhe. Zaituni Msofe-Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mhe. Bahati Henerico-Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na SACF. James John-Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa.
Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Kyerwa Mhe. Innocent Bilakwate amesema ataendelea kuisemea Wilaya ya Kyerwa katika ngazi ya juu ili iweze kusonga mbele huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Kyerwa katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved