Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe ametoa tuzo za ufaulu bora wa kidato cha sita mwaka 2024 kwa walimu kwa kuzingatia hali ya ufaulu katika masomo wanayoyafundisha.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya amewapongeza Walimu na watahiniwa wote waliofanya vizuri katika mtihani wao wa kidato cha sita kwa kupata daraja la kwanza.
Aidha amempongeza Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa SACF. James John kwa kuwa na utaratibu wa kuandaa hafla ya utoaji tuzo za ufaulu bora kwa walimu na wanafunzi kwani huongeza morali kwa walimu na wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao.
Hafla hiyo imefanyika katika Shule ya Sekondari Mukire, ambayo imeshika nafasi ya kwanza kiwilaya na kimkoa na nafasi ya 35 kitaifa, baada ya watahiniwa wote 45 kupata ufaulu wa daraja la kwanza (division one).
Shule hiyo imetunukiwa zawadi ya ngao ya ufaulu bora huku Mkuu wa Shule na walimu waliofaulisha katika masomo yao kwa wanafunzi kupata gredi A hadi C kutoka katika shule zingine nne za Serikali, walipokea tuzo za vyeti na fedha taslim. Aidha kwa kuzingatia pia ufaulu wa GPA kwa kila somo, walimu wanne wenye ufaulu wa juu, kupita wenzao, walipokea fedha taslim hadi shilingi laki saba kila mmoja.
Vile vile walimu wenye ufaulu bora kutoka shule zingine tano za Serikali zilizopo katika Wilaya ya Kyerwa ambazo ni; Isingiro, Nyabishenge, Kimuli na Mabira pamoja na shule mbili za binafsi za Kaisho na Kyerwa Bright Star walipokea tuzo za vyeti na fedha taslimu.
Awali akitoa taarifa ya ufaulu kwa ujumla, Afisa Elimu wa Wilaya Kyerwa Mwl. Ndabazi Stephano amesema, jumla ya shule saba zilifanya Mtihani wa Kidato cha Sita mwezi mei 2024 katika wilaya ya Kyerwa na matokeo ya watahiniwa wote wakipata Daraja la Kwanza na la Pili isipokuwa Mwanafunzi mmoja tu ndiye kapata Daraja la tatu.
“Kama Msimamizi wa idara, nawapongeza walimu na wanafunzi wote, kwa ufaulu mzuri, pia naipongeza OR Tamisemi kwa kubuni mkakati wa kusimamia shule kwa malengo mahsusi, yaani Key Performance Indicators (KPIs), Mkakati uliozaa matunda nchi nzima.
Kwa dhati, naishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za ujenzi wa miundombinu iliyopelekea Wilaya ya Kyerwa kusajili shule 10 za Kidato cha Tano na Sita ndani ya miaka miwili tuu, yaani mwaka 2021/22 na 2022/23.” Ameeleza Mwl. Ndabazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa SACF. James John amewapongeza walimu na wanafunzi kwa ufaulu mzuri na ameahidi kuendelea kushirikiana na walimu, wazazi na wadau wa elimu ili kuongeza chachu ya ufaulu na hivyo kufikia matakwa ya mahiri zilizokusudiwa katika mitaala ya elimu.
Vile vile ameipongeza Bodi ya Shule na Jukwaa la Wazazi wa shule hiyo kwa kuendelea kujitolea na kuunga mkono juhudi za Serikali kwa Kuajiri walimu wa muda 20 na kujenga nyumba ya walimu ya two in one yenye thamani ya milioni 75.
Protenes Alexander, muhitimu wa Kidato cha sita 2024 ambaye amepata Division one ya point 6 amewashukuru walimu kwa ufundishaji na kazi kubwa waliofanya kuwafundisha na kuwaomba kuendelea na moyo huo huo huku akiwasihi wanafunzi wanaoendelea na masomo kuongeze bidi katika masomo yao.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kyerwa ambaye alitoa zawadi ya shilingi Milioni moja, Diwani wa Kata ya Kikukuru, Wenyeviti wa Bodi ya Shule, wazazi, Maafisa Elimu Kata wa Kata zote, wakuu wa shule za sekondari, na viongozi wa Chama cha Walimu Wakuu wa Wilaya ya Kyerwa na Mkoa wa Kagera pamoja na wageni mbalimbali.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved