Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Flanklin Rwezimula leo Septemba 14, 2023 amefanya ziara ya kutembelea Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA katika Wilaya ya Kyerwa na kuwahimiza wasimamizi na wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo.
Ametoa rai hiyo baada ya kutembelea mradi huo wenye thamani ya Bilioni tatu ambao umeanza kutekelezwa Juni Mwaka 2023 na bado upo katika hatua ya Msingi.
Dkt. Rwezimula amewataka wasimamizi wa Mradi huo kuhakikisha wazabuni wanaongeza kasi kwa kuanza kuleta vifaa vya ujenzi kama mawe, kokoto na mchanga, huku akiwataka mafundi wakuu kuongeza mafundi wadogo ili kazi ya ujenzi ianze mara moja.
Aidha amewataka wasimamizi wa mradi huo kutoa mrejesho katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kushirikiana na Ofisi ya Mkugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ili kuweza kusaidiana katika kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi huo, Mthibiti Ubora wa Shule Bw. Damian Barabona amesema mradi huo umekuwa na kasi isiyoridhisha kwa sababu ya changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa mafuta na kuchelewa kwa simenti na nondo ambazo tayari tarehe Septemba 12, 2023 wamepokea vifaa vya kuanza ujenzi ikiwemo mifuko ya simenti 1,800 na nondo 950 huku mafundi wote wameitwa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo mara noja.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved