Kamati ya Elimu ya Afya ya Msingi katika Wilaya ya Kyerwa imefanya kikao chake leo tarehe 15 Septemba 2023, kwa ajili ya kujadili mpango wa kampeni ya kitaifa ya utoaji wa chanjo ya matone ya Polio itakayotolewa kwa watoto wa umri chini ya miaka nane kuanzia tarehe 21 hadi 24 Septemba mwaka huu.
Akiongoza kikao cha kamati hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka wanakamati kutoa elimu kwa wazazi na jamii kwa ujumla ili waachane na dhana potofu kuwa chanjo hizo zinamadhara kwa Watoto kiafya.
Amewataka wanakamati kuwa mabalozi kwa kutoa elemu kwa jamii na kuwaeleza faidi za chanjo kwa kuwa Wilaya ya Kyerwa iko mipakani mwa nchi, na jamii isipoondokana na dhana potofu inaweza kukaribisha madhara.
“Kila mmoja akilibeba hili, na kila taasisi wabebe hili na waende kwa watumishi walioko chini, tuelezane kila mtumishi atakuwa na familia na kila familia itakuwa na marafiki, tukawe mabalozi na tukifanya hivyo tutakuwa ‘tumekava’ sehemu kubwa.” Amesema Mhe. Msofe.
Awali akiwasilisha taarifa katika kikao hicho Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Dkt. Lewanga Msafiri amesema kampeni hii imelenga kuwafikia Watoto 95,545 na wamepokea dozi 115,000 ya chanjo ya polio ambayo itatumika katika zoezi hilo.
Aidha amesema mafunzo yameshaanza kutolewa kwa wahudumu wa afya na yataendelea kutolewa kwa wahudumu wengine na wasimamizi wa kampeni, huku zoezi la utoaji elimu kwa jamii likiendelea kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo ya Habari, mikutano katika nyumba za ibada.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved