Mashindano ya Michezo ya Shule za Msingi Tanzania ngazi ya Wilaya yamezinduliwa katika Shule ya Msingi Nkwenda katika Kata ya Nkwenda Wilaya ya Kyerwa.
Akifungua mashindano hayo Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewataka wanafunzi wanaoshiriki katika mashindano hayo kujituma na kufanya vizuri katika ngazi zote watakazoshiriki, ikiwa ni pamoja na kudumisha nidhamu na utii katika mashindano hayo.
“mkawe mabalozi wazuri, wenye nidhamu na utii mtakapokuwa kwenye makambi ya Wilaya, Mkoa na Taifa ili kulinda jina la Wilaya yetu na kuiletea ushindi” ameeleza Mhe. Msofe.
Aidha amewataka wazazi kulinda na kuendeleza vipaji vya watoto wao, huku akitoa rai kwa waalimu kuendelea kuibua na kulea vipaji vya watoto katika Wilaya ya Kyerwa.
Awali Afisa Michezo wa Wilaya ya Kyerwa Ndg. Daima Nkinda amesema kuwa mashindano hayo yameanza tangu mwezi Februari mwaka huu kwa kuhusisha timu za madarasa kwa madarasa ili kuunda timu za shule na baadae kuunda timu ya Kata.
Baada ya hapo ziliundwa timu za Tarafa na leo zimeshindana kuunda timu ya Wilaya ya Kyerwa ambayo itaenda kushiriki mashindano ya Mkao tar. 26 Mei 2024 katika chuo cha Ualimu Katoke kilichopo Wilaya ya Muleba Mkoa Kagera.
Michezo inayoshindaniwa ni pamoja na Mpira wa Miguu, mpira wa pete, mpira wa wavu, riadha, ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya pamoja na miruko ya juu na chini.
Kauli mbiu ya UMITASHUMITA mwaka 2024, Miaka 50 ya UMITASHUMITA Tunajivunia Mafanikio Katika Sekta ya Elimu, Michezo na Sanaa, Hima Mtanzania Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved