Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe leo Oktoba 31, 2023 amefanya mkutano wa hadhara na wananchi katika Kata ya Kibingo ikiwa ni mwendelezo wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Wilaya ya Kyerwa.
Katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi wa Kata ya Kibingo kuacha kuhujumu miundombinu ya maji kwa kung’oa na kuchoma moto mabomba ya maji, huku akiahidi kufanya uchunguzi na kufuatilia uharibifu huo na watakaobainika watashughulikiwa kisheria.
Amesema serikali inatumia fedha nyingi kuwapelekea wananchi miundombinu ya maji hivyo inawalazimu wananchi kuitunza na kuwa walinzi wa miundombinu hiyo kwani ikiharibiwa watakaoathirika ni wananchi.
Amewasisitiza wananchi wa Kata hiyo kuendelea kujiandikisha na kujaza fomu pamoja na kufuata taratibu za kupata vitambulisho vya taifa vya NIDA na leo katika Kata hiyo amegawa vitambulisho 728 kwa wananchi ambao walishajiandikisha.
Vile vile amesema serikali inaandaa utaratibu wa kuwakopesha fedha wananchi ambao watahitaji ili waache kuuza kahawa ikiwa bado iko shambani na badala yake waisubiri mpaka ikauke na baada ya kuvuna na kuuza kahawa yao watalipa deni lao, ikiwa ni njia ya kukomesha magendo ya kahawa katika Wilaya ya Kyerwa.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya aliambatana na Katibu Tawala wa Wilaya, wataalamu mbalimbali kutoka TARURA, RUWASA, NIDA, Viongozi wa Ulinzi na Usalama pamoja na wataalamu kutoka Halimashauri ya Wilaya ya Kyerwa.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved