Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amepokea mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (Cooperate Social Responsibility- CSR) wa Mradi wa Kufua Umeme wa Kikagati katika Kikao kilichofanyika leo Aprili 16, 2024 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Afisa Kiungo Jamii wa Mradi huo Bi. Jacqueline Stewart amesema, kwa mwaka huu wamepanga kutekeleza shughuli mbalimbali za Uwajibikaji kwa Jamii ili kuendelea kusaidia jamii inayozunguka mradi huo na kutengeneza mahusiano mazuri na jamii hiyo.
Bi Jacqueline amesema wamepanga kutoa huduma za elimu kwa jamii katika suala la usalama barabarani pamoja na usalama wa raia dhidi ya ukatili kwa kushirikiana na jeshi la polisi ili kupunguza ajali na vifo vinavyosababishwa na vyombo vya moto pamoja na ukatili wa raia unaotokea mara kwa mara katika jamii inayozunguka mradi huo.
Vile vile amesema watakuwa na programa ya afya kwa kutoa elimu juu ya kupima Maambuzi ya Virusi vya UKIMWI, ikiwa ni pamoja na kupima magonjwa ya kansa, TB na shinikizo la damu kwa lengo la kuimarisha afya za wananchi wa eneo hilo.
Pamoja na mambo mengine pia amesema wanaendelea na zoezi la uchakataji wa hati miliki za ardhi kwa wananchi nane wa upande wa Tanzania waliohamishwa katika maeneo yao na kupata sehemu nyingine ili waweze kuyamiliki kihalali ikiwa ni pamoja na Kuongeza huduma za maji kwa kushirikiana na RUWASA, pamoja na utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo hayo.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewashukuru kwa mipango mizuri na ambayo itawasaidia wanakyerwa kwa kuwa salama hasa katika elimu ya usalama barabarani na elimu ya usalama wa raia ambayo itatolewa kwa jamii ya wanakyerwa wanaozunguka maeneo ya Mradi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa pamoja na Wataalam mbalimbali kutoka ofisi za umma katika Wilaya ya Kyerwa.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved