Kamati ya Elimu ya Afya ya Msingi imefanya kikao chake leo tarehe 25 Oktoba 2023, kwa ajili ya kujadili mpango wa kampeni ya kitaifa ya utoaji wa chanjo ya matone ya Polio awamu ya pili itakayotolewa kwa watoto wa umri chini ya miaka nane kuanzia tarehe 2 hadi 5 Novemba mwaka huu
Akiongoza kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Katibu Tawala wa Wilaya Bw. Mussa Gumbo ametoa wito kwa jamii kushiriki ipasavyo katika kuhakikisha watoto wao wenye umri chini ya miaka nane wanapatiwa chanjo hiyo.
Aidha imeishukuru jamii ya Kyerwa kwa kushiriki kikamilifu katika chanjo ya awamu ya kwanza kwa kusema, “Niendelee kuwashukuru sana wazazi, niendelee kuishukuru jamii ya Kyerwa kwa kujitokeza kwenye ile awamu ya kwanza mpaka kufikia lengo. Hii inaonekana ni namna gani Watanzania na Wanakyerwa tunaufahamu mkubwa kuhusiana na maswala mbalimbali ikiwemo maswala ya afya.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico amewasihi wahusika kuwa waadilifu na kushirikiana kikamilifu ili kufanikisha zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kutumia nyumba za ibada na kuwashirikisha Watendaji wa Kata na Vijiji kwani wao wanaijua jamii na wanaweza kusaidia katika kuihamasisha ishiriki kikamilifu.
Awali akitoa taarifa ya chanjo awamu ya kwanza iliyofanyika mwezi Septemba mwaka huu na taarifa ya maandalizi ya kampeni ya Dkt. Shafii Mzirai amesema kampeni ya awali walipata mafanikio makubwa kwa kuchanja watoto 122,760 sawa na asilimia 128% Zaidi ya lengo ambalo walijiwekea la kuchanja watoto 95,454 katika Wilaya ya Kyerwa.
Dkt. Shafii amesema kamati imejipanga kwa kuanza kutoa matangazo mbalimbili pamoja na kuunda timu ya watu 849 ambao watashiriki katika zoezi la utoaji chanjo na tayari wamepokea fedha kiasi cha shilingi 179,975,000 ambazo zimetolewa na serikali kuu.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved