Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtambulisha kwa Wananchi na kumkabidhi eneo la mradi Mkandarasi Kampuni ya Shandong Luqiao Group atakayeanza ujenzi wa barabara ya Kyerwa - Omurushaka (km 50) kwa kiwango cha lami na kumuagiza Wakala ya Barabara (TANROADS) kumsimamia Mkandarasi huyo ili barabara hiyo ikamilike kwa wakati bila ya kusuasua.
Hafla ya kumkabidhi Mkandarasi imefanyika leo 18 Oktoba 2024 katika eneo la Rwenkorongo Wilaya ya Kyerwa ambapo Bashungwa ameeleza ujenzi wa barabara utaziunganisha Wilaya za Karagwe na Kyerwa kwa kugharamiwa na Serikali kwa Shilingi Bilioni 94.34.
“Mheshimiwa Rais anatambua wanaKyerwa walikuwa na kiu kubwa na barabara hii ndio maana ametoa kibali ili niweze kufika hapa na kumkabidhi Mkandarasi huyu kwenu ili aweze kuaza ujenzi na kuwaondolea wananchi kero ya usafiri mliyokuwa mnaipata”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia Mkandarasi kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo iliyokuwa inaishia Kata Chonyonyo na kuunganisha kipande cha kilometa 11 hadi kufika Omurushaka ambapo TANROADS wanaendelea na taratibu za kimkataba.
Amesisitiza kuwa ujenzi wa barabara ya Kyerwa - Omurushaka utafungua fursa mpya za Kibiashara, Uchumi na Uwekezaji pamoja na kuchochea shughuli za utalii katika Mbuga za Taifa za Ibanda, Burigi Chato, Rubondo na Rumanyika zilizopo katika Mkoa wa Kagera na Geita.
Aidha, Bashungwa amebainisha mikakati ya Serikali ya kuendelea kuifungua Wilaya ya Kyerwa kwa barabara za lami ambapo ameeleza barabara Omurushaka - Kyerwa itakuwa na mwendeleo hadi Murongo (Km 112.11) na kuunganisha Mji wa Nkwenda na Nyakaiga pamoja na kupendezesha mji wa Isingiro na Nkwenda kwa barabara za lami.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa huo ikiwemo Sekta ya Afya, Elimu, Kilimo na Miundombinu ya barabara.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved