Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa limeridhia kupitisha rasimu ya bajeti ya Shilingi 50,329,376,863.00 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambayo sawa na ongezeko la 14.9% ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo Halmashauri ilipitisha kiasi cha shilingi Bilioni 42.8 ambayo inaendelea kutekelezwa.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe ameipongeza Halmashauri kwa kuandaa bajeti ambayo imegusa Nyanja zote za maendeleo na kutoa wito kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kasi ili kutoa huduma kwa wananchi huku akiitaka Halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato.
“Tuna kila sababu ya kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika vyanzo tulivyo navyo, lakini pia tuna kila sababu ya kuendelea kubuni vyanzo vingine vipya vya kuendelea kuongeza mapato.” Amesema Mhe. Msofe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico amesema bajeti hiyo itaenda kutekelezwa kama ilivyopangwa kwani atahakikisha anasimamia utekelezaji wa bajeti hiyo kama alivyosimamia bajeti zingine zilizopita ili kuendelea kuijenga Kyerwa.
Awali akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu Ndg. John Msafiri, amesema Halmashauri inakadiria kupokea na kutumia jumla ya shilingi 50,329,376,863.00 kutoka katika vyanzo vya; mapato ya ndani shilingi 6,060,197,120,00 Ruzuku ya Serikali shilingi 37,450,477,743.00 na fedha za nje (Wahisani) 6,818,702,000.00 ambazo zitatumika katika kutekeleza shughuli za Halmashauri.
Aidha, Ndg. Msafiri amesema vipaumbele vya bajeti hiyo ni kujengea uwezo watumishi, Kuboresha shughuli za kilimo, Kusimamia mazingira na mabadiliko ya Tabia ya nchi, Kuwezesha ukusanyaji wa mapato na Kuboresha ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kyerwa Mhe. Innocent Bilakwate ameipongeza Halmashauri kwa kuandaa mpango mzuri wa Bajeti na kusema atasimamia na kuhakikisha bajeti hiyo inapitishwa katika ngazi zote zinazofuatia za Mkoa na Bunge.
Nao Waheshimiwa Madiwani wameonesha kuwa na imani na kuunga mkono mipango na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwemo Baraza la wafanyakazi, kamati ya ukimwi, kamati ya elimu, kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira, kamati ya fedha, Utawala na mipango.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved