Mkutano wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa umefanyika leo tarehe 08 Novemba 2024 kwa ajili ya kujadili taarifa ya utekelezaji wa robo ya kwanza, kuanzia mwezi Julai hadi Septemba 2024/2025.
Mgeni rasmi wa Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe ametoa rai kwa wananchi waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kupiga kura ili kuwapata viongozi watakao waletelea mafanikio katika jamii zao na kufanya mikutano ya kampeni ya kistaarabu.
“Nitoe rai kwa wananchi wote wa Kyerwa tuliojiandikisha tukakamilishe lengo la kujiandikisha kwetu, tukakamilishe haki yetu ya msingi kwenda kuwachagua viongozi tunaoona watatuvusha, viongozi waliobora katika jamii zetu.
“Waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa Kisiasa mko hapa mnanisikia twendeni tukahamasishe wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kutimiza haki yao ya kidemokrasia wakachague viongozi watakaoona wao ni bora katika jamii zao.
“Pia tunaenda kwenye kampeni, kama kiongozi wa ulinzi na usalama wa Wilaya, niwaombe sana ndugu zangu wanasiasa tukafanye siasa za kistaarabu, uchaguzi na kampeni wala sio vita, tukumbuke kuna maisha baada ya uchaguzi, tukumbuke kwamba sisi ni ndugu mmoja, isifike mahali tukatengeneza uadui kwa sababu tunaenda kufanya uchaguzi, hapana! uchaguzi upo kwa mujibu wa sharia lengo ni kuchagua viongozi lakini kutimiza haki ya kikatiba” amefafanua Mhe. Msofe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico akisoma taarifa yake kwa Mgeni rasmi amesema Halmashauri Kyerwa inaendelea na usimamizi wa miradi mingi inayotekelezwa kupitia fedha za mapato ya ndani na fedha kutoka Serikali Kuu ili iweze kutoa huduma zenye tija katika jamii.
Aidha ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Kyerwa ikiwa ni pamoja na miradi ya afya, elimu, maji, barabara na umeme.
Pamoja na shukrani hizo, baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wakichangia katika baraza hilo wameelezea juu ya uwepo wa changamoto ya maji katika kata zao na kuomba zishughulikiwe ili kuwakwamua wananchi wa maeneo yao.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved