Mkutano wa baraza la Madiwani kwa robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 katika Halmshauri ya wilaya ya Kyerwa umefanyika leo tar. 10 Novemba 2023 katika ukumbi wa Rweru Plaza ulioko katika Wilaya ya Kyerwa.
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amesema haridhishwi na utendaji kazi wa Mkandarasi wa Kampuni ya JAMTA Costruction Investiment Ltd Vumwe Jeneral Service and Supplies Co. Ltd. inayotekeleza miradi mikubwa miwili ya maji katika Wilaya ya Kyerwa ambayo ni Nkwenda, Runyinya Chanya utakaohudumia kata tatu za Nkwenda, Rwabwere na Iteera pamoja na mradi wa Kaisho Isingiro.
“kinachoonekana hapa ni changamoto ya mkandarasi kutucheleweshea sisi kazi yetu ya kupata huduma kwa wananchi… kama mradi wa Kaisho Isingiro ni wa siku nyingi lakini tukisikiza historia sioni kama anania ya kututekelezea huu mradi. Kwa sababu msimamizi ni BUWASA, niseme sasa RUWASA wasiliana na BUWASA lakini pia na Mkandarasi aje ofisini kwangu,” Amesema Mhe. Msofe.
Kwa upande Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mhe. Bahati Henerico amesema Wanakyerwa wanaungana na Mkuu wa Wilaya kwa kutokuwa na imani na Mkandarasi huyo kwani wananchi hawana maji na kumtaka Menaja wa RUWASA Wilaya ya Kyerwa Eng. Shukrani Tungaraza kuchukua hatua za kuacha naye.
Akichangia hoja hiyo, Diwani wa Kata ya Nyakantuntu Mhe. Issa Katunzi amesema Mkandarasi wa miradi hiyo Mikubwa ya maji hawafai wananchi wa Kyerwa kwa kukosa uzalendo wa kutekeleza majukumu yake na anatakikwa kukatishwa mkataba na kuwaomba Waheshimiwa Madiwani wengine kuungana ili kutafuta suluhisho la swala hilo.
Akifafanua hoja hiyo Meneja wa RUWASA Eng. Shukrani Tungaraza amesema Mkandarasi huyo hajaongezewa muda na anatakiwa kukatwa asilimia 0.1% kwa muda wa siku mia moja na akishindwa kumaliza mradi huo atakuwa amevunja mkataba huo, na kuwaomba waheshimiwa madiwani kuwa wavumilivu kidogo ili akishindwa kumaliza kwa siku zilizobaki watavunja mkataba.
Kwa upande mwingine baraza hilo limempongeza Mkuu wa Wilaya na Vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Kusimamia oparesheni ya kuzuia magendo ya kahawa ambayo yamepelekea makusanyo makubwa ya mapato ya ndani.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved