Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tar. 25 Aprili 2024 katika Wilaya ya Kyerwa umefanyika mdahalo maalum wenye mada mbalimbali zinazohusiana na muungano.
Wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, TARURA, RUWASA, TANESCO, TAKUKURU, TFS na Jeshi la Polisi waliwasilisha mada mbalimbali ambazo zilichangiwa na washiriki wa mdahao huo huku wanafunzi wakitoa burudani mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe amewashukuru watumishi na wananchi kwa kushiriki kikamilifu maaadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia kwenye usafi wa mazingira na kupanda miti katika Shule ya Sekondari ya Kyerwa Modern, Kushiriki Dua na sala maalum, Michezo mbalimbali na uzinduzi wa chanjo katika Kata ya Isingiro, kushiriki usafi, kupanda miti na kutembelea wagonjwa katika Kituo cha Afya Nkwenda na kumalizia na mdahalo wa leo.
Aidha amesema kuna changamoto nyingi zimeshughulikiwa na zipo zinazoendelea kushughulikiwa ikiwemo barabara ya lami ya Omurushaka-Rwenkorongo ambayo tayari imesainiwa na muda wowote mkandarasi ataanza kazi ya kuitengeneza.
Vilevile amewataka Wanakyerwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Sita kwa kuendelea kutunza miundombinu ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ili iwezee kuinufaisha jamii ya sasa na vizazi vijavyo.
Pia amewataka Wanakyerwa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, kutunza mazingira kwa kupanda miti pamoja na kulinda Amani na usalama wa nchi.
Baada ya mdahalo huo, Mkuu wa Wilaya alijumuika na wananchi katika kufuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mubshara katika viwanja Rwenkorongo Kata ya Kyerwa.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru inasema, “miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu.”
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved